Kabla ya mwaka 1981 waumini wa kisabato waliokuwa wanaishi sehemu ya mwenge walikuwa wanakwenda kusali huko Magomeni Mwembechai kila Sabato na kwa wakati wote . Ndipo ilipofika mwezi Juni mwaka 1981 uongozi wa kanisa la Ma Gomeni waliona vyema kuanzisha kundi katika sehemu ya Mwenge. Waliona ni rahisi kwao ku Sali Mwenge ili kujipunguzia safari ndefu na nauli za mabasi kwenda Magomeni.

Baraza la Kanisa chini ya Mchungaji John Moses lilikutana na kukubaliana kuanzisha kundi la Mwenge sehemu hii na kumchagua Zephania Gesogwe kuwa Mkuu wa kwanza kwenye kundi hilo. Kundi hilo lilikuwa likisali kwenye shule ya jeshi la wananchi ambapo ndipo shule ya Makongo High School ilipo leo. Baada ya kuanza kundi hilo waumini wa kundi la zamani la Lugalo wakaungana nao. Wakati huo waumini takribaani ya 20 walikuwepo lakini wakati huu ni familia moja tu ingali ipo hapa Mwenge.

Katika mwaka 1982 waumini hao walipata matatizo ya kusali siku za Jumamosi kwani shule ilikuwa inatumia madarasa hadi jumamosi. Hivyo kundi liliombwa kutafuta sehemu nyingine ya kuabudia. Ndipo walihamia na kusali kwenye shule ya Msingi ya Mwenge na kuanza kuendesha ibada zao bila wasiwasi. Lilipo hamia shule ya MSINGI YA MWENGE likawa linaongozwa na Tumaini Mtana. Katika miaka hiyo baadhi ya madarasa yalitumika kwa shule siku ya jumamosi hivyo kelele ziliendelea kutawala wakati ibada ya siku ya sabato ikiendelea. Pia iliwapasa waumini kuwalinda watoto wasiharibu maua ya shule au kuharibu madawati. Zaidi ya hapo haikuwa rahisi kuwa na ibada za Jumatano, kufungua na kufunga Sabato kwani marazingine wanafunzi walikuwa wakiyatumia madarasa wakati huo. Baadaye waumini waliongeezeka na kufurika chumba cha darasa walilokuwa wanatumia kwa ibada, hivyo baadhi yao wakawa wanabaki nje wakati wa ibada. Hivyo ilipofikia Machi 23, 1983 Kundi la Mwenge liliamua litafute kiwanja ili kuliwezesha kujenga jengo la muda wakati wanafanya mpango wakujenga Jengo la kudumu.

Juhudi za kupata eneo la kanisa hazikuwa rahisi kwani maeneo ya serikali yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya madhehebu mbalimbali yalishachukuliwa na madhehebu mengine. Lakini kwa azma ya mbingu ilibidi hili litekelezwe Zab. 118:5. Washiriki waliamua kufunga na kuombma ili kupata kiwanja. Sheria ya Kijiji cha Mwenge kilichomiliki viwanja vya Mwenge iliruhusu wanakijiji wasio pungua 10 kuomba kiwanja kwaajili ya michezo au maendeleo yao wenyewe wanaoishi kijijini. Kutokana na utaratibu huo waumini wa dhehebu la kisabato waliokuwa na nyumba kwenye kijiji cha Mwenge waliorodhesha majina yao na namba za nyumba zao na kupeleka ombi kuwa wao wakiwa wanakijiji hawa na mahali pa kumwabudu Mungu. Majina ya waumini hao ni kama ilivyoorodheshwa hapo chini:

Jina la Muumini Namba ya nyumba alipoishi
1. Alinanine O. Mwambogela Na.114
2. Neema Mwakisopile Na.5
3. Asaph Ndaro Kisama (marehemu)   Na.109
4. Dr Josiah Salehe (Marehemu) Na.108
5. John A. Nyika(Marehemu) Na.355
6. Eliud Omeme Na.31
7. D. Bandoma Na.40  
8. Amos Mwakalinga   Na.220
9. Josephat Machunde Na.72
10. D. Masamba Na.161
11. Clementina Onyango Na.204
12. A. Musiba Na.308
13. E. Mshana Na.249

Wote hawa waliweka sahihi zao kwenye barua ya maombi kuomba kiwanja hicho Katika maombi hayo waliomba eneo la kutosha kujenga jengo la kanisa nyumba ya kuishi Mchungaji, nyumba ya zahanati, nyumba ya kuishi mganga wa zahanati na nyumba ya kufundishia watoto wadogo. Kutokana na maombi hayo hapo Septemba 15, 1985 wakaruhusiwa kupata kiwanja kilichopo hapa kwenye eneo letu la kanisa.

Kutokana na hayo waumini wa Mwenge waliamua kwa pamoja kutoka shuleni na kuhamia kwenye kiwanja chao. Jambo la kwanza waliloamua lilikuwa kujenga banda la miti na matope la kuabudia lenye urefu wa futi 55 na upana wa futi 25. Banda hilo liliezekwa kwa mabati 36. Mwaka 1986 walianza kuabudu kwenye banda hilo. Baada ya kuingia kwenye banda hilo wakafanya mpango wa kupima kanisa la kudumu. Mipango ilipokamilika jengo la kudumu lilianza kujengwa mwaka 1987. Hivyo ujenzi huo uliomalizika mwaka 2002 ulichukua muda wa miaka 15 kukamilika.